Mtibwa kuwakaribisha KMC kesho (J’mosi)
Mtibwa kuwakaribisha KMC kesho (J’mosi)
Baada ya kufanikiwa kukusanya pointi 9 katika mechi tatu wana tam tam kesho (Jumamosi) wanashuka tena uwanjani kuwakaribisha KMC katika mchezo wa ligi kuu bara (TPL) unaotarajiwa kufanyika katika uwanja wa Manungu, saa 10:00 jioni.
Kikosi cha wana tam tam chini ya Zuber Katwila kimekuwa kikifanya maandalizi ya mchezo huo katika uwanja wake wa nyumbani Manungu, tayari wachezaji walio katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Salum Kihimbwa na Kelvin Sabato Kongwe wamejumuika na wenzao mapema leo kwa ajili ya mchezo huo wa kesho.
Huo utakuwa mchezo wa 9 katika ligi kuu bara kwa upande wa Mtibwa Sugar huku mechi nne zote za nyumbani wana tam tam wakifanikiwa kuibuka na ushindi katika mechi zote za nyumbani.
Wana tam tam wamefanikiwa kukusanya pointi 16 katika michezo 8 huku wapinzani wao KMC ya jijini Dar es salaam wakiwa wamekusanya pointi 8 katika michezo 8 ya ligi kuu bara.
Wana tam tam wataingia katika mchezo wa kesho wakiwa wanaongoza msimamo wa ligi kuu bara baada ya kukusanya pointi 16 katika michezo 8 mbele ya Azam Fc ambao wanashikilia nafasi ya 2 baada ya kukusanya pointi 15.

Post a Comment